Kauli ya Rais Kikwete yawakera maaskofu | Send to a friend |
Monday, 06 June 2011 21:08 |
0diggsdigg Boniface Meena JUMUIYA ya Kikristo Tanzania (CCT), imempa Rais Jakaya Kikwete saa 48 ikimtaka awataje hadharani viongozi wa madhehebu ya dini aliosema wanahusika na biashara ya kuuza dawa za kulevya na kwamba asipofanya hivyo itakuwa ni aibu kiongozi huyo wa taifa. Makamu Mwenyekiti wa CCT, Askofu Dk Valentino Mokiwa alisema hayo jana wakati jumuiya hiyo ilipokuwa ikitoa maazimio ya Mkutano wa 45 wa Halmashauri Kuu ya jumuiya hiyo.Askofu Mokiwa alisema kauli ya Rais Kikwete imewasikitisha kwa kuwa amewahusisha viongozi wote wa dini jambo ambalo si zuri mbele ya jamii. " Rais ataje majina ni kina nani wanahusika na ndani ya saa 48 awe ameyataja la sivyo itakuwa ni aibu zaidi kwake na serikali," alisema Mokiwa.Alisema wanategemea Rais Kikwete atafanya hivyo na kinyume chake atakuwa hajawatendea haki wananchi. Akihutubia waumini wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mbinga, juzi kwenye ibada maalumu ya kupewa daraja la Uaskofu na kusimikwa Mhashamu Askofu John Ndimbo wa jimbo hilo, Rais Kikwete aliwaonya viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini nchini akiwataka kuacha tabia ya kushiriki biashara ya kuuza dawa za kulevya, badala yake washirikiane na viongozi wa serikali katika kudhibiti biashara hiyo haramu. Alisema kuwa baadhi ya viongozi hao wa dini wamekuwa wakishiriki kufanya biashara ya dawa za kulevya kwa kuwafanyia mipango vijana kuwatafutia hati za kusafiria kwenda nchi za nje kwa ajili hiyo. “Inasikitisha sana na kutisha. Biashara hii haramu sasa inawavutia hata watumishi wa Mungu, taifa letu litaharibika tusipokuwa makini katika hili, baadhi yenu tumewakamata,” alisema. Msimamo juu ya Katiba Mpya Akisoma tamko lao baada ya mkutano wa Halmashauri Kuu wa 45, Mwenyekiti wa CCT, Askofu Peter Kitula alisema jumuiya hiyo imeitaka serikali kusimamia kwa umakini suala la Katiba Mpya hasa katika ukusanyaji wa maoni. Alisema kuwa ukusanywaji huo wa maoni kwa wananchi na makundi yote ya kijamii ni muhimu ukafanywa na chombo huru. "Kazi hii isiharakishwe na wala isicheleweshwe. Yafaa iwe imekamilika mapema ndani ya muda wa kadri kabla ya kuanza kwa mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015," alisema. Askofu Kitula alisema kuwa serikali inapaswa kuangalia ufa uliopo kati wananchi wa kawaida na wale wenye nacho kwani unazidi kupanuka na kuibua matabaka."Hali hii inasababisha malalamiko miongoni mwa wananchi dhidi ya serikali yetu. Malalamiko na ukweli huu umechukuliwa na wadau wa vyama vya siasa kufanya maandamano ambayo yamekuwa yakiwavutia wananchi wengi." Alisema hali hiyo inachangia hali ya kisiasa kuwa tete hasa ikilinganishwa na baadhi ya nchi jirani ambako bei ya mafuta iko chini zaidi ya Tanzania na nchi hizo zinapitisha mafata hayo hapa."Serikali isahihishe jambo hili pasipo kuchelewa. Vyama vyote vya siasa vihamasishe wananchi kuleta maendeleo bila kujadi itikadi za vyama vyao." Askofu Kitula alionya kuhusu siku za ibada na kutaka ziheshimiwe na watu wote na mamlaka zote. Alisema ni vyema serikali isipange matukio muhimu ya kitaifa kama uchaguzi mkuu na uchaguzi wa serikali za mitaa siku za ibada. "Kadhalika, wahadhiri na wakufunzi wa vyuo vikuu, vya elimu ya juu na taasisi zake wasiwapangie wanafunzi mitihani au mazoezi ya vitendo siku za ibada," alisema Askofu Kitula. CCT yazungumzia tiba asilia Kuhusu tiba asilia, CCT imetoa wito kwa serikali kusaidia katika utafiti na matokeo yake yawekwe bayana ili kuwaondolea wananchi hofu ikiwa ni pamoja na huduma zitakazothibitishwa kupatikana mahali pengine nchini. "Kadhalika, serikali isimamie utunzaji wa mazingira ili miti na mimea mingine yenye vyanzo vya tiba asili istawi na kupatikana muda wote," alisema Askofu Kitula.Aidha, CCT imesisitiza msimamo wake kutaka mambo ya kuendesha shughuli za dini yatenganishwe na mamlaka ya kuendesha nchi. |
No comments:
Post a Comment